Journal of Kiswahili Studies (JSS) ni jarida lenye matoleo mawili kwa mwaka lililoanzishwa kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Pwani na TUSIMA (RISSEA), na kufadhiliwa na Prof. Rajab, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Pwani. Jarida hili lilianzishwa kwa minajili ya kukuza na kuendeleza utafiti na utaalamu wa lugha ya Kiswahili kwa kuwapatia watafiti wa taaluma mbalimbali, hasa za lugha ya Kiswahili, Fasihi na Utamaduni, nafasi ya kuchapisha matokeo ya tafiti zao.
JSS, ni jarida ambalo makala yake hudurusiwa kwa uhakiki na uhariri wa upofu ili kuhakikisha uzito wa kiakademia wa makala unadumishwa. Ni matumaini ya Mhariri kwamba wasomi wa majarida yetu watanufaika mno kwa elimu iliyomo katika makala ya jarida hili na vile vile ni matumaini yetu kwamba watafiti wengi wengine watahamasika kwa kusoma majarida yetu na kutuma makala ya tafiti zao ili yachapishwe.
Ijapo kwa sasa jarida hili linachapisha makala ya Kiswahili, Fasihi na Utamaduni hatutasita kufungua milango ya makala ya taaluma nyengine za kisayansi, kiteknolojia na kielimu kwa Kiswahili endapo wapendwa na wasomi wetu watapenda tufanye hivyo kwa kutujulisha kupitia maoni yao kwa Mhariri Mkuu.